Kenya:Rais Kenyatta aongoza Wakenya kuanza kuutazama mwili wa kigogo Kibaki

Kenya:Rais Kenyatta aongoza Wakenya kuanza kuutazama mwili wa kigogo Kibaki

RAIS Uhuru Kenyatta analiongoza taifa leo Jumatatu kumpa heshima zake za mwisho, Rais mstaafu Mwai Kibaki aliyefariki Ijumaa wiki jana.

Tayari, mwili wa kigogo Kibaki umepelekwa katika majengo ya bunge.

Unahifadhiwa katika makafani ya Lee, kitengo cha watu mashuhuri na chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa kijeshi, KDF.

Ulisafirishwa bungeni kupitia gari la hadhi la kikosi cha jeshi.

Rais Kibaki aliongoza Kenya kati ya 2003 – 2013, na akiwa Amiri Jeshi Mkuu Mstaafu atazikwa chini ya mila, tamaduni na itikadi za jamii ya wanajeshi.

Aidha, mizinga 19 itafyatuliwa.

“Yatakuwa mazishi ya kitaifa, Rais Mwai Kibaki amefanyia taifa hili mengi makuu,” akasema Rais Kenyatta, akitangaza rasmi kifo cha mwendazake, Ijumaa.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i ambaye anaongoza kamati ya usalama kutayarisha maziko ya mwendazake amethibitisha atapumzishwa mnamo Jumamosi, nyumbani kwake Othaya, Kaunti ya Nyeri. Ibada ya wafu itafanyika Ijumaa.

Rais Kenyatta, akifuatwa na naibu wake, Dkt William Ruto na viongozi wengine wakuu serikalini, atafungua jamvi la Wakenya kuutazama mwili wa Kibaki, shughuli inayotarajiwa kuendelezwa kwa muda siku tatu.

Kifo cha Rais huyo wa tatu wa Jamhuri ya Kenya, kilijiri mwaka mmoja na nusu baada ya mtangulizi wake, Daniel Arap Moi kufariki Februari 2020.

Rais Moi alizikwa nyumbani kwake Kabarak, Kaunti ya Nakuru.

Marehemu Kibaki anakumbukwa kwa miradi mikuu kama vile ujenzi wa barabara kuu ya Thika – Nairobi, Thika Super Highway, uzinduzi wa masomo bila malipo katika shule za msingi za umma, kubuni nafasi za kazi kwa vijana kupitia sekta ya bodaboda, miongoni mwa mingine.

Kumuomboleza Shujaa hadi atapozikwa, idara zote za serikali na za kibinafsi zinapeperusha bendera nusu mlingoti.

Taifaleo

Asante kwa kushiriki!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *