Tanzania: Makonda aripoti kituo cha karibu asema Polisi Dar

Tanzania: Makonda aripoti kituo cha karibu asema Polisi Dar

Muliro alisisitiza umuhimu wa Makonda kuripoti polisi, akisema kwa sasa mifumo ipo ya kushughulikia masuala hayo, hivyo hata akiripoti kesi yake kwa maandishi itashughulikiwa.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemwambia aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuripoti tuhuma alizozitoa kwenye mitandao ya kijamii akidai kutishiwa maisha yake hadi kituo cha karibu.
Wito huo umetolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alipokuwa akizungumza na Mwananchi Jumanne Aprili 12.
“Sijazungumza naye (Makonda), lakini kupitia vyombo vya habari, namshauri aende kituo chochote cha polisi iwapo tuhuma alizotoa ni za kweli,” alisema.
Muliro aliongeza: Inategemea (Makonda) anaishi wapi, lakini aende kituo cha polisi kilicho karibu ili kutoa maelezo zaidi juu ya tuhuma alizozitoa.
Siku chache zilizopita katika ukurasa wake wa Instagram, Makonda aliandika ujumbe uliokuwa na kichwa cha habari “Nafahamu kuwa kuna makundi matano yamepangwa kuharibu maisha yangu.”

Katika ujumbe wake, Makonda alitaja makundi hayo kuwa ni pamoja na wauza dawa za kulevya na walengwa wao, mashoga na wale wanaotaka kulipiza kisasi dhidi yake.
Makonda pia alidai kufahamu mbinu zinazofanywa za kumuua kwa manufaa ya familia zao lakini pia kutoa mashahidi wa uongo kumfungulia mashtaka ya uhujumu uchumi.
“Kuna mambo mawili, pamoja na kazi nzuri nilizofanya kwa chama changu (CCM) na kwa wananchi wenzangu wa Dar es Salaam je hizi ni zawadi?”
“Hakika ukiwa mja muaminifu uliyetetea haki ya mafakiri na ukitoka katika familia masikini. Haya ndiyo malipo? ” Makonda alihoji katika ujumbe wake.
Aliongeza: Mtu aliyejenga hospitali, ofisi za walimu na za chama, vituo vya polisi, shule za sekondari na msingi, alinunua magari kwa ajili ya Jeshi la Polisi, alitibu wagonjwa bure kiasi cha kuleta madaktari wageni kutibu watu hapa Tanzania, leo, Ninaonekana kama ninafaa kunyongwa hadi kufa.
Aidha, alisema kuna kundi mtandaoni limelipwa ili kuwaandaa Watanzania pindi atakapokamatwa watatoa ushahidi dhidi yake.
“Ipo siku walemavu, yatima, wajane na wale wanaotamani watoto wao wasife kutokana na dawa za kulevya sauti zao zitasikika,” aliandika.
Alipotafutwa na Mwananchi kujua ni hatua gani amechukua dhidi ya vitisho hivyo, Makonda hakutoa jibu sahihi, badala yake aliambatanisha na ujumbe huo alioutuma kwenye Instagram.
Hata hivyo, Muliro alisisitiza umuhimu wa Makonda kuripoti polisi, akisema kwa sasa mifumo ipo ya kushughulikia masuala hayo, hivyo hata akiripoti kesi yake kwa maandishi itashughulikiwa.
“Ni jukumu letu polisi kuchunguza malalamiko yoyote ya jinai, lakini suala linalochunguzwa lazima liwe na ushahidi wa kutosha. Narudia iwapo madai yake ni ya kweli basi aende kituo cha polisi kilicho karibu,” alisema.
Hii si mara ya kwanza kwa Makonda kuibua tuhuma kupitia mitandao ya kijamii, Machi aliandika kwenye akaunti yake ya Instagram akimtaka mfanyabiashara Ghalib Said Mohamed (GSM) kuacha mali yake kwenye kiwanja Na.60, Regent Estate kilichopo Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Asante kwa kushiriki!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *